
MALENGO
- Onesmo Frank
- May 14, 2020
- 3 min read
KABLA HAUJAANZA SAFARI, JIULIZE KWANZA “NINATAKA KWENDA WAPI?”
Siku za karibuni nilikutana na rafiki yangu mmoja hivi aliyekuwa anahitaji nimuelekeze jinsi ya kuomba ufadhili wa masomo nchi za nje. Kwakuwa Nina uzoefu wa kutosha kuhusu fadhili za masomo, niliona sio mbaya nikamsaidia mdogo wangu huyu angalau kwa kumpa maarifa. Nikiwa nimejiandaa kuzungumza naye kwa mapana na marefu kuhusiana na fadhili za masomo, nilimuuliza, “kwahiyo, umepanga kwenda kusoma nini nje ya nchi?” Alinijbu, “kwakweli sijui nataka kwenda kusoma nini ila nataka kwenda kusoma masters nje ya nchi”. Nilishusha pumzi kisha nikaamua kumwambia ukweli, “mdogo wangu, hatua ya kwanza kabisa, naomba uende ukakae chini ujiulize ni kitu gani unataka kwenda kusomea, baada ya hapo tutaendelea. Kwa ninavyofahamu, hakuna atakayekulipia kwenda kusoma kama hata wewe mwenyewe haujui unataka kwenda kusomea nini”.
Hii ni changamoto ya watu wengi, waliosoma na ambao hawajapata bahati ya kwenda shule. Mara nyingi huwa tunajikuta hatujui tunataka kufanikisha nini katika maisha yetu. Wengi hua tunatamani mafanikio lakini hatujui tunataka kufanikiwa kiasi gani, mwishowe tunajikuta tunahangaika tu kwenye maisha. Wataalam wa maendeleo huwa wana msemo wao kwamba “kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa”.
Ndugu zangu, Safari ya mafanikio ni kama Safari nyingine zozote zile. Kabla haujatoka nyumbani na begi lako; kabla haujapanga nguo kwenye begi; kabla haujatafuta nauli; kabla hata haujaaga ndugu na jamaa, ni lazima kwanza ujue unataka kwenda wapi. Ukishajua unakotaka kwenda, itakuwa rahisi kwako kujua utafute nauli kiasi gani, utatumia muda gani kufika, ubebe nguo kiasi gani lakini pia utajua ni usafiri gani utatumia. Juzi nilibishana kidogo na wadau kwenye Facebook walipokuwa wanasema “vijana wengi tunasumbuliwa na umaskini kwasababu hatuna mtaji”. Nililipinga na kusema, ingawa mara nyingi huwa ni rahisi kusema hatuna mitaji, uhalisia wake ni kuwa wengi wetu hatuna malengo; hatujui tunataka kufanikisha nini. Japo wengi wetu huwa tunasema hatuna mitaji, ukitushtukiza na swali kama “unahitaji mtaji kiasi gani?” Au “nikikupa mtaji kiasi hiki utafanya biashara gani?” Wengi huwa tunashindwa kujibu haya maswali na kuishia kusema “ningepata pesa kidogo, ningefungua biashara” au “ah, kwa kunipa pesa hiyo naweza kufungua duka au kuuza nyama au kufungua mgahawa au biashara yoyote ile”. Majibu kama haya ni ushahidi tosha kwamba tatizo letu wengi sio kukosa mtaji bali ni kukosa malengo. Hata kama una hela, hauwezi kutoka asubuhi ukaenda stendi kununua ticket bila kujua unataka kwenda wapi. Vivyo hivyo kwenye maisha, hauwezi kufungua tu biashara wakati haujui unataka kufanikisha nini. Kwa kukosa malengo, mara nyingi tunajikuta tunapoteza fedha ambayo pengine tungekuwa tumeweka malengo, tungeizalisha mara dufu.
Tunatakiwa kufanya nini?
Kuanzia leo, tujaribu kuweka malengo, na uzuri ni jambo jepesi sana. Chukua kalamu na karatasi yako kisha gawanya katika sehemu tatu. Sehemu ya kwanza andika malengo ya kiuchumi, sehemu ya pili andika malengo ya kielimu na sehemu ya tatu andika malengo ya ki jamii. Ukishamaliza, tuliza akili yako kisha angalia maisha yako kuanzia ulikotoka mpaka sasa. Jiulize, ninahitaji kufanikisha nini kwenye maisha yangu? Ninahitaji kupata nini kwenye maisha yangu? Kama leo ndio ingekuwa siku yangu ya mwisho kuishi duniani, je ningejilaumu kwakuwa sikufanikisha nini? Ninataka kuwa mtu wa aina gani miaka kumi ijayo? Ukishafikia hii hatua, anza kuandika kwenye karatasi hayo mambo unayotaka kuyafanikisha. Katika hatua hii usiogope kitu chochote wala usiangalie changamoto gani zinakuzunguka. Weka malengo makubwa kabisa, jinsi ya kufanikisha ni hatua nyingine tutaikuta huko mbele. Wengi huwa tunatingwa na hali ya maisha inayotuzunguka na kujikuta tunaogopa kuweka malengo tunayoyatamani. Biblia imetuambia kwamba, penye nia pana njia lakini pia kuna sehemu nyingine inasema mwanadamu akiweka malengo, Mungu ataongoza hatua zake. Kwahiyo tunatakiwa kuweka malengo makubwa kabisa tukiwa na imani kwamba tutayafanikisha. Weka malengo ambayo yatakutisha, malengo ambayo yatakunyima usingizi, malengo ambayo yatakunyima raha, malengo ambayo yatakufanya uyawaze muda wote. Mtu mmoja aliwahi kusema, “kama malengo yako hayakuogopeshi, hayakunyimi usingizi; kuna uwezekano sio makubwa vya kutosha”. Marehemu Ruge aliwahi kusema “unapoota ndoto, oya ndoto kubwa kama jua ili ukilikosa jua upate mwezi”. Anza kwa kuota ndoto kwanza, mengine yote yatafuata.
OTA NDOTO; IPIGANIE NDOTO YAKO
WEWE NI MSHINDI
Onesmo Mushi
https://onesmofrenk.wixsite.com/website
https://www.facebook.com/PIGANIANDOTOYAKO
コメント