
SABABU YA MAPAMBANO
- Onesmo Frank
- May 24, 2020
- 1 min read
NI IPI SABABU YAKO YA KUPAMBANA?
Nilikuwa nasoma kitabu kimoja leo nikakutana mstari mmoja mzuri sana. Ulisomeka hivi, “mtu mwenye sababu ya kupambana kamwe hawezi kukata tamaa”.
Huu mstari ulinikumbusha Nelson Mandela, akiwa magereza kwa miaka 27 alikuwa anapiga push-up mia na hamsini kila siku, anafanya mazoezi ya kukimbia bila kusogea kwa dakika arobaini kila siku, anaendelea kusoma sheria na vitabu vingine kila siku. Hata maaskari magereza walipokuwa wakimnyanyasa, Nelson alificha hasira yake. Hata pale hali ilipokuwa ngumu kabisa, Mandela alijaribu kuvumilia na kuonesha kwamba yupo fiti ingawa kiuhalisia hali ilikuwa tete. Mandela alikuwa akisema, kamwe haitakiwi kumuonesha adui udhaifu wako. Adui akikuona una ujasiri yeye mwenyewe anakosa nguvu. Mandela alikuwa na msemo wake ukisema “hata pale unapoona mambo yamekuwa magumu kabisa, kamwe usiinamishe kichwa chini. Nyayua kichwa chako juu ukiliangalia jua na miguu yako ikiendelea kusonga mbele.” Mandela alisema ni lazima amshinde adui kwa sababu ya nchi yake, ni lazima avumilie ili kumtia nguvu mke wake Winnie aliyekuwa anamtembelea kwa miaka 27, ni lazima apambane kwasababu ya watoto na mama yake.
Je wewe ndugu yangu, ni nini sababu ya mapambano yako? Ni kipi kitakutia nguvu pale ambapo changamoto za maisha zitakupiga na kukulazimisha kukata tamaa? Ni kipi kitakachokwambia amka tusonge mbele hapa sio mwisho??
Sababu ya kupambana ni muhimu sana kwenye kupigania ndoto zetu. Kila mmoja wetu ajiulize ni nini kitakachomchochea kupambana hata pale mambo yatakapokuwa magumu. Nini kitakachomtia nguvu na kumyanyua hata pale atakapokuwa ameishiwa nguvu? Hasira za mafanikio zinahitaji sababu.
IPIGANIE NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO
WEWE NI MSHINDI.
Onesmo Mushi
https://onesmofrenk.wixsite.com/website
https://www.facebook.com/PIGANIANDOTOYAKO
Comments