AMINI KATIKA UNACHOKIFANYA
- Onesmo Frank
- May 4, 2020
- 3 min read
AMINI KATIKA UNACHOKIFANYA; KIONGEZEE THAMANI
Kwa wengi wetu tumekuzwa na fikra kwamba ili uweze kufanikiwa, basi unalazimika kufanya kazi za aina fulani. Unahitajika kuwa mhandisi au daktari au mfamasia au mhasibu au mtaalam fulani anayefanya kazi kwenye ofisi kubwa binafsi ya serekali. Jamii na elimu yetu kwa ujumla imetujengea hii hofu kiasi kwamba tunapokosa fursa za kusomea kozi kama za sheria, udaktari, uhandisi nk, moja kwa moja tunajiweka kwenye kundi la walioshindwa. Kwasababu ya fikra hizi tunajikuta tunazizika ndoto zetu na kuanza kuishi maisha ya kubangaiza, yanayoendana na yale jamii inayoyaamini. Ukitaja kazi fulani isiyo na kipato kikubwa, kila mtu anavuta picha ya mtu maskini, mlevi, aliyekata tamaa, mwenye madeni nk. Hapana, hizi ni fikra potofu tunazotakiwa kuzibadilisha. Haijalishi unafanya kazi gani wala una elimu kiasi gani, unaweza kuwa vyovyote vile unavyotaka kuwa. Cha kufanya ni kimoja tu; USIKUBALI KUWA WA KAWAIDA. “Take it to the next level.”
Gokce raia wa Uturuki maarufu kama “Salt Bae”, ni moja wapo kati ya vijana maarufu sana duniani kwa sasa. Kijana huyu alizaliwa 1983 na aliacha shule akiwa darasa la tano. Akiwa na umri wa miaka 13, Gocke alianza kufanya kazi kwenye bucha katika kitongoji chao. Baada ya muda, kijana huyu alianza kufanya kazi kwenye mgahawa na kujifunza mapishi. Alianza kuweka mbwembwe kwenye mapishi yake; namna anavyokata nyama, vitunguu, nyanya na viungo vyote. Baada ya muda, Gocke alifungua mgahawa wake katika kitongoji chao. Mwaka 2017, Gocke alituma video ya sekunde 37 Instagram ikionesha ujuzi wake wa mapishi na kukata viungo. Wakati wa kuhudumia wateja, Gocke alikuwa na mbwembwe za kumkatia mteja nyama aliyoichoma kwa umahiri mkubwa. Siku moja mfanye biashara mmoja mkubwa nchini Uturuki alivutiwa na madoido ya Gocke hivyo akaenda kula pale mgahawani. Baada ya kuona nia na utayari wa huyu kijana, mfanyabiashara yule alimua kuwekeza kwenye biashara ya Gocke na kuipanua; yaliyofuata baada ya hapo ni historia. Ndani ya kipindi cha miaka mitatu, Gocke ameshafungua migahawa kwenye miji yote mikubwa duniani kuanzia Manhattan NewYork mpaka Dubai, Paris, London, Madrid nk. Sahani moja ya nyama ambayo pengine haifiki hata kilo mbili, inauzwa zaidi ya laki tatu za kitanzania. Pamoja na kuwa milionea kwa sasa, Gocke bado ni mpishi kwenye moja ya migahawa yake. Migahawa hii utawakuta watu maarufu wa dunia, wacheza mpira kama Neymar, Benzema, Lewandowski, wana mziki maarufu kama Dj Khalid, P.Didy, Jay Z na wengine kibao wanahudhuria migahawa yake ili tu kufurahia mbwembwe za huyu kijana.
Unaweza kuona kama ni muujiza kufanya hivi au bahati; la hasha. Ni maamuzi ya kuamini katika ndoto yako, kukiongezea thamani kile unachokifanya ili kuwa tofauti na wengine na kuamua kupambana asilimia 120% ili kuzifanikisha ndoto zako. Tuna mifano mingi sana Tanzania ya watu waliopambania ndoto zao bila kujali jamii inawaonaje na wala inasemaje. Vijana hawa kama wakina Diamond, Millard Ayo, Masanja, Joti, Mpoki, Maulid Kitenge, Mbwana Samatta, Majizo na wengine kibao wanafurahia maisha kwa sasa.
Usikubali kuishi maneno ya watu. Wengi watakwambia haiwezekani kwasababu hii na ile, lakini mtu pekee mwenye kuamua iwezekane au isiwezekane ni wewe binafsi. Ukiamua kwamba utafanikiwa basi hakuna la kukuzuia na ukikubali pia kuwa hauwezi kufanikiwa basi hapatakuwa na wakukuzuia. Haijalishi ni kazi gani unaifanya wala una elimu kiasi gani; hatua ya kwanza ni kuamua; kuamua kuamini kwamba inawezekana. Baada ya hapo mengine yote ni matokeo ya kujiamini kwako. Hali yako ya sasa ni matokeo ya fikra na matendo yako; ukitaka kuibadilisha ni lazima uanzie kwenye fikra.
IPIGANIE NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO. WEWE NI MSHINDI.
Author: Onesmo Mushi
Comments