
ANZA NA KIDOGO
- Onesmo Frank
- Jun 6, 2020
- 2 min read
KITUMIE KIDOGO ULICHONACHO; MUNGU ATAKUONGEZEA MBELE YA SAFARI
Wengi wetu huwa tunazidiwa na hofu na kuogopa kuanza kutembea kuelekea kwenye ndoto zetu tukiamini kuwa tulichonacho hakitoshelezi. Hii imetufanya kuendelea kuishi maisha ya kimaskini tukisubiri mambo yakae bila kujua kuwa mambo hayatokaa yakae Sawa bila mimi na wewe kuamua kuanza kuyaweka Sawa.
Nikisoma Biblia yangu Samweli wa kwanza 17, inatuonesha kijana mdogo ambaye hakuwa na silaha za kisasa wala mwili mkubwa lakini alikitumia kidogo alichokuwa nacho kufanya mambo makubwa. Daudi alitumia kombeo tu na jiwe lakini alimwangusha Goliathi aliyekuwa na upanga, mwili mkubwa, ngao na mavazi ya kujilinda. Wakati wanajeshi wa Izraeli wakiogopa mwili mkubwa wa Goliathi, Daudi aliona kwa mwili ule siwezi kumkosa na kombeo. Silaha ndogo na duni aliyokuwa nayo, Mungu aliitia nguvu.
Nikisoma tena kitabu cha Kutoka, namuona Musa akitumwa na Mungu kwenda kwa Farao. Japo Musa alikuwa na aibu na asiyeweza kuongea mbele za watu, Mungu alimwagiza kukitumia hicho hicho kidogo alichonacho akimuahidi kumwongoza ya kusema mbele ya Farao aliyekuwa tishio. Tunaona huko mbele Mungu alimfanya Haruni kuwa msemaje wake na mwishowe wakafanikiwq kuwakomboa wana wa Izraeli. Uwezo kidogo aliokuwa nao, Mungu alimwongezea.
Mwaka 2017 nilipata kujifunza kwa kijana mmoja aliyeanzisha biashara mjini Morogoro kwa mtaji wa njaa yake. Akiwa hana chochote lakini anahitaji kula, alimuomba mzee mmoja angalau amtume/amwagize sehemu kisha amlipe ili aweze kupata hela ya kula. Baada kufanikiwa kutumwa na kulipwa shilingi 1000, aliwaza kuifanya hiyo kuwa biashara yake, biashara ya kutumwa. Baada ya muda mfupi jamaa alikuwa maarufu, yeye anatumwa kupeleka taarifa, anatumwa kupeleka watoto shule mikoani, anatumwa kushughulikia documents za biashara na nyingine mbalimbali makao makuu TRA, anatumwa kuishughulikia mizigo bandarini nk. Mpaka sasa huyu jamaa biashara yake inakuwa na kupanuka. Kwa njaa tu aliyokuwa nayo huyu jamaa, Mungu alimpa wazo la biashara.
Ndugu zangu, kaka, dada, mdogo na rafiki yangu, hicho hicho kidogo ulichonacho kinaweza kufanya mambo makubwa. Tuna mifano kadha wa kadha ya watu walioanzia kwenye vitu vidogo kabisa na sasa ni mabilionaire. Twende tukaanze kuuishi ndoto yetu. Mafanikio ni hatua, hicho kimoja ulichonacho ukikitumia inavyopaswa ndio vitafika viwili, vitatu mpaka mamia. Twende tukazitumie hizi talanta chache tulizopewa, tusikubali kuzifukia chini tukusubiri ziongezeke. Hakuna siku hali itakuwa Sawa, wala hakuna siku utapata vyote unavyovitaka, mtaji utaongezeka ukiwa katikati ya Safari. Kwa imani, tuanze kutembea kuelekea kwenye ndoto zetu.
Onesmo Mushi
https://onesmofrenk.wixsite.com/website
https://www.facebook.com/PIGANIANDOTOYAKO
Comentarios