
Kama unavyotafuta hewa
- Onesmo Frank
- Jun 6, 2020
- 1 min read
KAMA UNAVYOTAFUTA HEWA
Kuna bwana mdogo mmoja alikuwa anatamani sana kufanikiwa katika maisha yake ila hakujua apambane kiasi gani. Siku moja alimtembelea mzee mmoja aliyekuwa amefanikiwa sana, akamwambia mzee naomba unishauri nipambanaje, nipigane kiasi gani ili niweze kupiga hatua kama wewe. Mzee akamwuliza, ni kweli una nia ya kufanikiwa kwenye maisha yako? Kijana akajibu, ndio mzee, natamani sana kuondokana na haya maisha ya tabu.
Basi, mzee akamchukua kijana akaenda naye baharini, walipofika ufukweni akamwambia kijana amfuate. Mzee akaanza kuingia kwenye maji, kijana akashtuka kidogo kwasababu alikuwa amevaa suti yake safi kabisa. Akamwuliza mzee, mzee vipi tena mbona kwenye maji? Mzee akamjibu, kama unataka mafanikio nifuate. Basi kijana akaanza kumfuata mzee huku mzee akizidi kusonga. Kina kikazidi kuongezeka, kijana akaanza kuzama lakini mzee akaendelea kusisitiza amfuate. Baada ya muda kidogo kijana akazama akawa anarusharusha mikono kutafuta hewa.
Baada ya muda mfupi, mzee akamuokoa kijana akamrudisha nchi kavu, kijana akiwa hoi kabisa. Mzee akamuuliza kijana, ulipokuwa umezama ulijisikiaje? Kijana akajibu “NILICHANGANYIKIWA, NILIKUWA NAJITAHIDI KUFANYA CHOCHOTE KILE ILI NIPATE HEWA” Kijana akiwa amekasirika akamwambia mzee, mimi nilitaka mafanikio sio kuzama kwenye maji. Mzee alitabasam kisha akamwambia, UTAYAPATA MAFANIKIO IKIWA UTAPAMBANA KAMA ULIVYOKUWA UNAPAMBANA KUPATA HEWA WAKATI WA ULIPOKUWA UMEZAMA.
Kisha mzee akasimama akaondoka zake.
Onesmo Mushi
https://onesmofrenk.wixsite.com/website
https://www.facebook.com/PIGANIANDOTOYAKO
Comments