top of page
Search

Jiandae

JIANDAE KWA SAFARI

Mwezi wa Tisa Mwaka 2015, nilipokea ujumbe kutoka ubalozi wa Marekani ukinijuza nimechaguliwa kushiriki kwenye program fulani na kunihakikishia tarehe ya Safari. Sababu ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa kusafiri nje ya nchi, nilijikuta natumia muda mwingi sana kujiandaa na Safari. Nilianza kuandaa passport ya kusafiria pamoja na visa. Nilijikuta nikisoma muda mrefu kwenye internet ili kujua nini kinachoruhusiwa kwenye ndege na nini kisichoruhusiwa, begi lipi nibebe, vitu gani niweke, nguo gani nivae nk. Na ujanja wangu wote, ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa kufika uwanja wa ndege kwahiyo ilinibidi pia ni jifunze ni vitu gani vinafanyika pale. Nilisoma kwamba nitasachiwa, mizigo yangu itapimwa uzito na haitakiwi kuzidi kilo 23 kwa begi moja, nilijua kwamba begi langu la mgongoni halitakiwi kuzidi kilo saba na mengine mengi. Nilijifunza pia kwamba nitatakiwa kupita kwenye dirisha la uhamiaji kabla sijaruhusiwa kupanda ndege. Nilitumia muda mwingi kujifunza pia kwenye ndege kupoje, choo kipo wapi, niongeaje na muhudumu ili aniongezee chakula au kinywaji, nawashaje tv, nachezaje game na mambo kama hayo. Kwasababu nilitakiwa kuunganisha/kubadilisha ndege nchini Uswis, nilitumia muda mwingi pia kujifunza jinsi ya kutembea kwenye ngazi za lift, kwenye sakafu ambayo na yenyewe inatembea🤭, jinsi ya kusoma matangazo, jinsi ya kutafuta ndege yangu lakini pia jinsi ya kuunganisha internet ya airport. Ilipofika siku ya Safari, kama ungekutana na mimi wala usingejua kama ndio ilikuwa mara yangu ya kwanza kusafiri na ndege.

Ujumbe

Nimeshare simulizi hii ili kuonesha umuhimu wa maandalizi katika Safari ya ndoto zetu. Ukishaweka malengo (ukishajua unakotaka kwenda), hatua inayofuata ni kujiandaa na Safari. Wengi wetu huwa tunapata hasara na kupoteza fursa kwasababu huwa hatupo tayari kujiandaa. Mwaka 2016, kwasababu ya kutokujiandaa niliingia kichwa kichwa shambani nikijifanya ninajua mwishowe nikapoteza milioni 15, inaniuma mpaka leo.

Baada ya kuweka malengo, tunatakiwa kujiandaa ili tukianza Safari basi tuwe kwenye nafasi nzuri. Katika kujiandaa, mambo matatu yanashauriwa. Kwanza, kujiuliza ni wapi zilipo fursa za kukamilisha malengo yetu. Je ni shambani, bank, kwenye taasisi, shule, chuo au ni wapi unahisi unaweza kupata fursa ya kukamilisha malengo yako? Unaweza kuzitafuta hizi fursa kwa kusoma kwenye vitabu, au mtandao au hata kwa kuuliza watu waliofanikiwa kwenye eneo hilo. Hatua ya pili, ni kujiandaa kuzitumia hizo fursa. Kwa mfano, ukishajua kwamba fursa ya kuanzisha biashara ya ndoto yako ipo bank, basi unajiandaa kwa kutafuta taarifa za nini ufanye ili kupata huo mkopo. Bank watahitaji labda business plan, asset, hati nk. Ukishajua haya, unaviandaa hivi vitu ili kujihakikishia nafasi ya kuitumia hiyo fursa. Kama ni shambani, basi unaweza kuanza kutafiti utalima wapi, mazao gani, hayo mazao yanahudumiwaje, soko lake lipo wapi, lakini waliofanikiwa katika hili eneo wanafanya nini cha tofauti. Ni muda mzuri wa kujifunza kwa waliofanikiwa ili usipate hasara ambayo ungeweza kuiepuka kama ungeuliza. Kama ni ufadhili basi ni hivyo hivyo, huu ufadhili unapatikana wapi, wanahitaji watu wa aina gani, unandae viambatanisho vya aina gani lakini pia ujiandaeje ili kujihakikishia nafasi.

Hatua ya mwisho ni kuchukua hatua, kufanya chochote kilichopo kwenye uwezo wako ili kujihakikishia nafasi ya kuipata hiyo fursa. Kama umeshajua kuwa wanaotoa ufadhili wanawahitaji zaidi watu wanaojitolea kwenye jamii, ndio muda sahihi wa kuanza kujitolea kwenye jamii ili kujiongezea nafasi. Kama wanahitaji zaidi mtu mwenye kujua lugha za kimataifa walau mbili, ndio muda sahihi wa kuanza kujifunza lugha nyingine. Kama wanahitaji zaidi mtu anayependa kusoma, ndio muda sahihi wa kwenda kwenye ubalozi wao na kujiandikisha kwenye maktaba yao ili waendelee kukufahamu.

Huu ndio muda sahihi wa kuonesha njaa ya mafanikio ya ndoto yako. Kama ndoto yako ni kupata nafasi kwenye hiyo kampuni, sio muda sahihi wa kwenda kujitolea pale hata kwa kufagia ukijua unajitengenezea njia. Ndio muda sahihi wa kwenda na huyo bosi shambani kwake kila siku ili ujifunze, ili aone una uchungu na ndoto zako aweze kukusaidia. Ndio muda sahihi wa kwenda kwa huyo mtaalam wa biashara na kumuomba akuelekeze jinsi ya kuandika business plan. Ndio muda sahihi wa kununua kitabu na kuanza kusoma jinsi ya kuendesha biashara. Kwa vyovyote vile itakavyowezekana, huu ndio muda sahihi wa kuhakikisha kwamba fursa ikitokea mlango wowote, kamwe hainiruki. Usije ukakubali muda ukafika ukasema, “ningejua, ninge…….”, muda huo utakuwa umechelewa sana. Mafanikio siku zote huwafuata waliojiandaa.

IPIGANIE NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO

WEWE NI MSHINDI.

Onesmo Mushi

 
 
 

Recent Posts

See All
JE KUNA BAHATI KATIKA MAISHA?

JE KUNA BAHATI KATIKA MAISHA? Oprah Winfrey aliwahi kusema, hakuna bahati kwenye maisha wala hakuna anayefanikiwa kwa kubahatisha....

 
 
 
ANZA NA KIDOGO

KITUMIE KIDOGO ULICHONACHO; MUNGU ATAKUONGEZEA MBELE YA SAFARI Wengi wetu huwa tunazidiwa na hofu na kuogopa kuanza kutembea kuelekea...

 
 
 

Comments


Post: Blog2_Post

Subscribe Form

Thanks for submitting!

  • Facebook
  • Twitter
  • LinkedIn
  • Facebook

©2020 by Maabara Ya Maisha. Proudly created with Wix.com

bottom of page