NDOTO YANGU NI MUHIMU
- Onesmo Frank
- May 2, 2020
- 3 min read
NI LAZIMA NIFANIKIWE Mwaka 2006, mtayarishaji wa filamu maarufu duniani Mel Gibson alitoa filamu iliyojulikana kwa jina la APOCALYPTO (naamini watu wengi wanaitambua kwa majina tofauti tofauti yasiyo rasmi😂). Filamu hii inawazungumzia watu wa jamii ya Maya walioishi nchini Mexico miaka mingi sana iliyopita. Kulikuwa na kijiji kidogo katikati ya msitu mkubwa ambacho watu wake waliishi kwa kupendana sana. Ghafla usiku mmoja wanakijiji hawa walivamiwa na watu wa jamii ya Maya na kutekwa ili kwenda kutolewa kafara kwa miungu. Katika mapambano kabla ya kutekwa, kijana Jaguar Paw alifanikiwa kuwaficha mke wake aliyekuwa mjamzito wa karibu kujifungua na mtoto wake mdogo kwenye shimo kubwa. Baada ya hapo, Jaguar alirudi kusaidiana kupambana na maadui lakini mwishowe walizidiwa nguvu na kutekwa. Safari ya kwenda uhamishoni ilikuwa ngumu na yenye mateso makubwa. Wanakijiji walifungiwa nira shingoni kama watumwa lakini pia mikono ilifungwa na walilazimika kutembea umbali mrefu. Muda wote wa Safari, kijana Jaguar Paw alikuwa akusali na kuahidi kuwa ni lazima atoke salama katika hili ili arudi kuikoa familia yake. Baada ya kufika uhamishoni, utaratibu ulikuwa mmoja. Mateka mmoja baada ya mwingine alipandishwa kwenye mnara mrefu kisha kukatwa kichwa ili kuitolea miungu sadaka ya damu. Lakini hata ilipofika zamu ya Jaguar, bado aliamini hatokufa ingawa alishalazwa kwenye sehemu ya kukatia na mkataji tayari alishanyanyua shoka juu tayari kwa kukata. Lakini ghafla mwanga kama wa jua ulionekana angani ikiwa ni ishara kuwa miungu ilikuwa imeridhika na damu hivyo Jaguar Paw akaponea chupuchupu. Baada ya hapo mateka waliobaki walipelekwa sehemu maalum ambayo wanajeshi wa hii jamii walitumia kujifunza shabaha. Kila mateka aliachiliwa kukimbia kama umbali wa meta 100 kisha wanajeshi walitumia silaha zote za jadi kupima uwezo wao wa kuuwa kwa mbali. Japo iliruhusiwa kuwa ukiweza kutoka hapa upo huru, hakuna mateka yeyote katika historia aliyewahi kutoka salama katika eneo hili, kwani kulikuwa na maelfu ya maiti mwisho wa eneo. Mateka wote waliotangulia walikufa lakini Jaguar bado aliamini hatokufa ili akaiokoe familia yake. Kweli, ilipofika zamu yake alifanikiwa kukimbia mpaka mwisho bila kufa. Ingawa alichomwa mshale mgongoni, alikataa kukata tamaa akiwa na lengo moja tu la kuikoa familia yake. Wanajeshi waliona hii kama dharau hivyo kuamua kumkimbiza Jaguar ili kumuua. Jaguar alikimbia kwenye msitu mkubwa, wenye kila aina ya vikwazo. Kuna muda alizama kwenye matope mazito lakini alikataa kukata tamaa; kuna muda alikimbizwa na mnyama mkali, nyoka, nyuki, na wanajeshi lukuki wenye kila aina ya silaha za jadi lakini alijiambia “ni lazima nishinde ili nikaiokoe familia yangu”. Ilifika mahali Jaguar akaamua kutokukimbia na kupambana na wanajeshi mmoja baada ya mwingine mpaka alipofanikiwa kuwaua wote. Mvua ikiwa inanyesha kubwa, shimo linajaa maji, Jaguar alijikokota akiwa na uchovu na madonda makubwa lakini akiwa na sababu iliyomtia nguvu, sababu ya kuiokoa familia yake. Hatimaye kwa ushindi mkubwa alifanikiwa kumuokoa mke aliyejifungulia kwenye shimo pamoja na watoto wake wawili. Ujumbe Ndugu zangu, Safari ya mafanikio inahitaji kijidhatiti na kujikana nafsi kama Jaguar Paw. Ili kupambana na changamoto na kuhakikisha kuwa haukati tamaa, unahitaji kuwa na sababu itakayokutia nguvu na kukuamsha tena wakati ukianguka. Inaweza kuwa ni watoto wako ambao unatamani wawe na maisha mazuri baada ya kuishi kwa tabu muda mrefu; inaweza kuwa ni mama yako aliye hospital na hela inahitajika ili kuokoa maisha yake; inaweza kuwa ni uchungu wa kusumbuliwa na matusi ya mwenye nyumba kila unaposhindwa kulipa kodi; inaweza kuwa ni manyanyaso na dharau unazozipitia kutoka kwa ndugu zako na jamii kwa ujumla kwa sababu ya umaskini wako; inaweza kuwa ni uchungu wa kuishi chumba kimoja na kila kitu kama stoo, inaweza kuwa ni chochote kile unachokipitia. Haijalishi ni nini, hakikisha unakuwa na sababu itakayokufanya uamke tena unapoanguka, na kuendelea kusonga mbele kwa ujasiri ukiamini kwamba ni lazima ufanikiwe. Hata alipokuwa karibu kabisa kufa, Jaguar Paw bado aliamini ni lazima atoke salama ili akaiokoe familia yake. Hata itakapotokea umekumbwa na changamoto kubwa kiasi gani, sema ni lazima niishinde ili kuiokoa familia yangu; ili kujenga heshima kwenye jamii yangu; ili kuwapa elimu bora watoto wangu; ili kuidhibitishia jamii kuwa wewe ni mahindi. UKIANGUKA, AMKA KUNG’UTA VUMBI, FUTA MACHOZI, ENDELEZA MAPAMBANO. HATUTAKATA TAMAA MPAKA TUMEYAKAMILISHA MALENGO YETU. NDIO HAKUNA LAKUTUZUIA.💪💪💪💪💪💪 Mungu akutie nguvu. Author: Onesmo Mushi #Daraja-la-Mafanikio
Comments