NI VIGUMU KUMSHINDA MTU ASIYEKATA TAMAA
- Onesmo Frank
- May 6, 2020
- 2 min read
Japo nimekuja kumfahamu kipindi cha mwisho mwisho wa imahiri wake, Mimi nilikuwa mmoja kati ya mashabiki wakubwa sana wa Mike Tyson. Nakumbuka mwaka 2002, akipigana na Lewis, sikulala mpaka saa Tisa za usiku nikisubiri pambano ambalo hata hivyo Tyson alipoteza. Achana na hili, mwaka 1990 Tyson alikuwa kwenye ubora wake, akiwa amepigana mapambano 37 bila kupoteza hata moja (hapa tunazungumzia pambano la uzito wa juu duniani). Tyson alikuwa tishio, kila bondia alikuwa akimwogopa. Achilia mbali mazoezi na wepesi aliokuwa nao, Tyson alijua pia kucheza na fikra za wapinzani wake. Alijua jinsi ya kuwafanya wapinzani wake watengeneze hofu na kujikuta wanasahau kufocus kwenye pambano na badala yake wanamuwaza jamaa muda wote. Kwa Tyson ulikuwa ukifanya kosa moja tu, unajikuta umeshapigwa muda mrefu sana.
Mwaka 1990, Tyson alikutana na jamaa ambaye hakupewa nafasi ya kushinda hata kidogo. Tyson anasema, alikuwa anajiamini kiasi kwamba hakuona haja ya kucheza na akili za huyu jamaa. Douglas alikuwa na changamoto kadhaa, wiki tatu kabla ya pambano alifiwa na mama yake lakini alikuwa akisumbuliwa na changamoto nyingine ikiwemo ulevi na kadhalika. Lakini siku ya pambano, Douglas anasema aliamini anaenda kumpiga Tyson, bila kujali umahiri wala umaarufu wake. Haikuwa kazi ndogo, zilipigwa ngumi za kutosha lakini jamaa alikuwa hapigiki. Kwenye round ya nane, Douglas alipigwa konde zito akajikuta amelala chali. Refa akiwa anahesabu, Douglas anasema alimkumbuka mama yake aliyefariki, akakumbuka maisha ya hovyo aliyokuwa anaishi mwisho akajikuta nguvu imemjia ghafla, akasimama tena. Round mbili baadae zilibadilisha historia kabisa, Tyson alipigwa makonde mazito akajikuta chini tena bila hata uwezo wa kuamka tena. Huo ndio ulikuwa mwisho wa pambano, Tyson akipoteza mchezo wake wa kwanza kabisa kwenye maisha yake. Baada ya mechi Tyson alipoulizwa kilichotokea, alijibu “NI VIGUMU SANA KUMSHINDA MTU ASIYEKATA TAMAA.”
Ujumbe
Haijalishi utakutana na changamoto kubwa kiasi katika pilika zako, jitahidi kupambana bila kuchoka, fanya lolote linalowezekana upige hatua. Martin Luther anatuambia, “kama hauwezi kupaa basi kimbia; hauwezi kukimbia basi tembea; hauwezi kutembea basi tambaa, fanya lolote lile unaloweza kuzisogelea ndoto zako.” Kamwe usikubali kusimama, kamwe usikubali kukata tamaa.Maisha yakikupiga (kwasababu kuna muda utakutana na changamoto) ukumbuke maneno ya huyu mwamba Tyson, “NI VIGUMU KUMSHINDA MTU ASIYEKATA TAMAA” , kisha amka tuendelee na Safari. Wahenga wanasema, changamoto isiyokuua inakuongezea ujasiri. Kila changamoto utakayokutana nayo, kila changamoto utakayoitatua inakusogeza karibu zaidi na mafanikio yako. Les Brown anasema “kila HAPANA utakayokutana nayo inakusogeza karibu na NDIO” Itakuwa rahisi, hapana, itakuwa ngumu sana lakini wewe ni mshindi; wewe una akili kuliko hiyo changamoto. Hakikisha maneno yako mwisho yanasomeka “nilikutana na changamoto fulani nikaishinda ndio maana nimefika hapa” na sio “nilikutana na changamoto fulani ikanishinda ndio maana nakufa maskini😰😰”
IPIGANIE NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO
WEWE NI MSHINDI.
Author: Onesmo Mushi
https://onesmofrenk.wixsite.com/website
コメント