
NIDHAMU
- Onesmo Frank
- May 31, 2020
- 2 min read
WIKI IJAYO TUNAENDA DAR ššæššæ.
Naamini wengi mliokulia kijijini mtakubaliana na mimi katika hili. Mwaka 2000 baada ya shule kufungwa bibi aliamua kutupeleka Daresalaam wajukuu wote. Baada ya kutupa taarifa kama wiki moja kabla, sikuwa napata usingizi kabisa. Ilikuwa mara yangu ya kwanza kabisa kufika Dar, jiji nililokuwa naliona kwenye TV na kusikia kwenye redio tu. Muda wote kwa siku Sita nilikuwa naiwaza Safari, itakuwaje, nitavaa nini, nitabeba nini, maisha ya mjini yatakuwaje lakini la muhimu kabisa āsiku tukirudi kijijini watoto wenzangu watanionaješ.ā
Kama kuna kipindi niliwahi kuwa na tabia nzuri nyumbani basi ni hiyo wiki kabla ya Safari. Nilikuwa nikiamka mapema kabisa, nafagia uwanja, nafagia banda mbuzi, nakimbia kiteka maji mtoni, nafua nguo zangu, naoga mapema, kamwe siendi kuzurura mitaani na mengine mengi. Nilikuwa najitahidi kuonesha nidhamu ya hali ya juu ili bibi asije kubadili mawazo. Siku ya Safari niliamka saa Tisa za usiku, nikawasha moto na kuwapashia watu wote maji ya kuoga kisha nikawaamsha. šš yani ndoto ya kwenda Dar ilikuwa muda wote kichwani mwangu, sikuwa na uwezo kubisa wa kulala. šš
Leo nimekumbuka hii story nikafurahi sana. Nimejiuliza, hivi tungekuwa wapi sasa hivi kama tungekuwa tunajituma kama watoto au vijana wa kijijini wakiahidiwa kwenda Dar? Unaweza kuona nilikuwa na nidhamu kiasi gani mara baada ya kuahidiwa kwenda jijini. Naamini malengo na ndoto zetu zitafanikiwa sana endapo tutaamua kupambana kila siku, kwa furaha, nguvu na hari kama vile tumeahidiwa kwenda Dar. Daresalaam ya sasa ni ndoto zetu, tunahitaji kuonesha nidhamu ya hali ya juu ili kufanikisha Safari. Tunahitaji kujituma kutafuta maarifa, kuacha kupoteza muda, kuamka mapema na kutekeleza majukumu kwa kasi kabisa kila siku bila kuacha wala kuchoka. Kuepuka kwenda kuzurura kwa watu watakaotusababishia kuonekana wazembe na muda wote kuwekeza katika yale yatakayotusaidia kufanikisha ndoto zetu. Tukiweza kujishughulisha kwa moyo na uwezo wetu wote, jamii itatusaidia kufika Dar ya ndoto zetu.
IPIGANIE NDOTO YAKO; WEWE NI MSHINDI.
Onesmo Mushi
https://onesmofrenk.wixsite.com/website
https://www.facebook.com/PIGANIANDOTOYAKO
Comments