top of page
Search

NIDHAMU YA MAFANIKIO

Je tupo tayari kulipa gharama??

Tajiri mmoja nchini marekani aliulizwa, Je ni mbinu gani unatumia kupata mafanikio? Tajiri alijibu, “kupata mafanikio ni kazi nyepesi sana kama mtu atafuata hatua kuu tatu. Moja, kuweka malengo. Mbili, kujiuliza ni gharama gani yupo tayari kulipa ili kufanikisha hayo malengo. Na tatu, kulipa hiyo gharama haraka iwezekanavyo.” Mwandishi akamuuliza tena, “kwahiyo tufanye nini ili kufanikiwa?” Tajiri akajibu, “kwakweli sijui mfanye nini, ila nina hakika kwamba msipokuwa na nidhamu ya kuyafanya yale yanayotakiwa, kamwe hamuwezi kufanikiwa.”

Mafanikio ni matokeo ya matendo yetu ya kila siku, hakuna muujiza kwenye mafanikio. Tulisema huko nyuma, kila jambo unalolifanya leo lina mchango kwenye malengo yako. Mchango unaweza kuwa wa kufanikisha malengo yako au kukwamisha malengo yako. Watu wote wanatamani kufanikiwa, wote wanatamani kuishi maisha mazuri na kuondokana na mateso ya umaskini; lakini je ni wangapi wanayaishi matamanio yao? Ni wangapi kwenye matendo yetu tunaonesha dhahiri kwamba kweli tuna uchungu wa kuyapata mafanikio? Biblia kitabu cha Mathayo 7:15-16 inatuambia kwamba “mtawatambua kwa matendo yao”. Je unayoyafanya yanakupeleka kwenye malengo yako? Jinsi unavyotumia muda wako kuanzia asubuhi mpaka jioni, je mtu akikuona ataweza kusema unapambania mafanikio ya ndoto zako? Je marafiki waliokuzunguka wanakusaidia kuzifikia ndoto zako? Vipi matumizi yako ya fedha kidogo uliyonayo kwasasa, unadhani inakupelekea kufanikisha malengo yako?

Unapotaka kufanikiwa, ni lazima ukubali kuzitoa sadaka baadhi ya starehe za muda mfupi ili uweze kupigania maisha mazuri ya kesho. Yesu alipotoka kuomba aliwakuta wanafunzi wake wamelala, akawaambia “kesheni mkiomba”, ni lazima tuwe tayari kuushinda usingizi wa sasa ili tuweze kuja kulala vizuri baadae. Tusipokuwa na nidhamu ya mafanikio kwa sasa, muda wetu mwingi ambao tungeweza kuutumia kuyafanya yale yenye faida kwenye ndoto zetu, utaliwa na mambo yasiyokuwa na faida, utaliwa na mambo yanayokwamisha ndoto zetu. Muda unaoutumia kuchati Facebook na Watsap ungeweza kuutumia kujifunza jambo fulani linalohusiana na unachokifanya. Tafiti zinaonesha, kama ukiweza kusoma angalau kitabu kimoja kwa mwezi, baada ya miaka mitano, utakuwa kati ya 5% ya wataalam kwenye eneo lako. Siku hizi teknolojia imeturahisishia mambo sana, tuutumie muda wetu vizuri kwa faida ya ndoto zetu. Badala ya kupoteza muda mwingi kwenye magroup na page za udaku Facebook, tafuta page zitakazokupa maarifa ya kuzifikia ndoto zako. Badala ya kutumia MB zako kusikiliza mziki kutwa YouTube, tumia MB hizo kusikiliza mafunzo ya ujasiriamali; mafunzo ya kuendesha biashara; mafunzo ya kutunza fedha; mafunzo ya kukuendeleza na kukuongezea thamani katika Safari ya ndoto yako. Kila siku pambana kutafuta kitu kitakachokufanya kuwa wa kipekee kwenye eneo lako. Kwenye maisha ya sasa hauhitaji kwenda chuo ili kuelemika, elimu ipo kila mahali ni maamuzi yako tu. Badala ya kutumia muda mwingi kwa umbea na mambo yanayozilisha fikra zako taarifa zisizokuwa na faida, tumia huo muda kutengeneza urafiki na yule aliyefanikiwa, tumia muda mwingi kujifunza kutoka kwake. Katika biblia tunaona Elisha alipokuwa anatumia muda mwingi kujifunza kwa Eliya. Eliya alipotwaliwa, Elisha aliweza kuyafanya yote aliyoyafanya Eliya, alijifunza na akawa nabii.

Tumia fedha kidogo unayoipata sasa kuwekeza kwenye ndoto yako. Badala ya kununua pakti ya sigara au bia, angalau mara moja toa shilingi elfu tano nunua kitabu. Hiki kitabu kitakusaidia wewe mama ntilie kujifunza pishi fulani litakaloleta utifauti kwenye biashara yako; hiki kitabu kitakusaidia wewe mchoma nyama ukagundua mbinu mpya ya kuwahudumia wateja wako; kitakufunza mbinu za kuongeza mavuno kwa wewe mkulima. Tumia kidogo ulichonacho kulipia semina na mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali na uhamasishaji yatakayokusogeza karibu na ndoto zako. Huo muda unaoutumia kuangalia TV upunguze kidogo uwekeze kwenye kujifunza mbinu za kutatua changamoto ukikutana nazo. Ndugu zangu, mafanikio yanaacha alama. Tukiwa tayari kuwa na nidhamu na kufanya yale yanayotakiwa, hakuna chochote kitakachotuzuia. Ndoto zetu zinatutaka tukubali kuwa watumwa kwa sasa ili kesho tuishi maisha tunayoyataka. Ni ngumu sana hapa mwanzo lakini tukiweza kujilazimisha na kufanya haya walau kwa miezi miwili, kichwa chako kitazoea na ghafla itageuka kuwa tabia yako. Hauwezi kufanikiwa kama muda wote umekaa baa unalewa, muda wote umekaa kwenye kijiwe cha kahawa, muda wote umekaa kusimanga na kuwasema wengine, muda wote unasikiliza mziki kwa lengo la kujiburudisha, muda wote umekaa kulalamika, muda wote umekaa kujadili siasa. Yabadilishe matendo yako, jifunze kuwa na nidhamu ya kuyafanya yale yote yanayotakiwa kufanya ili kufanikisha ndoto zako hata pale ambapo haujisikii kuyafanya. Kwa bahati mbaya sana, kamwe hautoweza kuifikia ndoto yako kama hautakubali kubadilika. Ifike mahali tuseme, “nimechoka kuishi maisha ya aibu, ninataka kubadilika, nataka kufanikisha ndoto zangu, nataka kuwa mwenye mchango katika jamii yangu”.

Itakuwa ngumu lakini faida yake ni kubwa; ni lazima tupambane kuvishinda vishawishi. Hauwezi kutaka kupunguza mwili wakati unaendelea kula vyakula vile vile vya mafuta. Ni lazima ukubali kujinyima; ni lazima upambane kuishinda tamaa ya mwili. Ni kweli utapishana na vingi sana kwa sasa lakini kuna siku utaangalia nyuma na kusema, “ama kweli nilifanya maamuzi ya busara.” Hata wewe unaweza kulala hotel ya nyota ukipumzika na mkeo badala ya vibanda umiza🤔, hata wewe unaweza kusafiri na kwenda kuangalia mpira ulaya kama wengine, hata wewe unaweza kuipeleka familia yako mapumzikoni kwenye fukwe za Brazil na Marekani, hata wewe unaweza kuwapeleka watoto wako Disney land, hata wewe unaweza kuiendesha hiyo gari unayoiota kila siku, hata wewe unaweza kusoma hicho chuo unachokiota kila siku, hata wewe unaweza kusafiri na ndege badala ya basi, hata wewe unaweza kuishi kwenye hilo jumba la kifahari, hata wewe unaweza kuheshimika kwenye jamii yako; lakini haya yote na mengine unayoyatamani yatabaki kuwa ndoto kama hautoamua kubadilika na kuwa na nidhamu ya mafanikio. Ukitaka kubadilisha maisha yako, anza kwa kubadili tabia yako. Ndoto yako ina thamani kubwa, usiiache ipotee kirahisi kwasababu ya starehe za muda mfupi.

IPIGANIE NDOTO YAKO; WEWE NI MSHINDI.

Onesmo Mushi

 
 
 

Recent Posts

See All
JE KUNA BAHATI KATIKA MAISHA?

JE KUNA BAHATI KATIKA MAISHA? Oprah Winfrey aliwahi kusema, hakuna bahati kwenye maisha wala hakuna anayefanikiwa kwa kubahatisha....

 
 
 
ANZA NA KIDOGO

KITUMIE KIDOGO ULICHONACHO; MUNGU ATAKUONGEZEA MBELE YA SAFARI Wengi wetu huwa tunazidiwa na hofu na kuogopa kuanza kutembea kuelekea...

 
 
 

Comments


Post: Blog2_Post

Subscribe Form

Thanks for submitting!

  • Facebook
  • Twitter
  • LinkedIn
  • Facebook

©2020 by Maabara Ya Maisha. Proudly created with Wix.com

bottom of page