ONDOA PLAN B
- Onesmo Frank
- May 5, 2020
- 2 min read
CHOMA HILO DARAJA; IPIGANIE NDOTO YAKO
Tafiti zinaonesha kuwa wengi wetu tunashindwa kuzipigania ndoto zetu kwasababu tunaishi kwa hofu. Wataalam wanasema, tunaingia kwenye mapambano tayari tukiwa tumeshaweka PLAN B vichwani mwetu, jambo linalosababisha tusipambane kikamilifu. Kwa mfano, unakuta mtu anafungua duka halafu anajisemea “ah, Ngoja nijaribu, ikishindikana si basi, ili mradi Nina kazi yangu” au mwingine anasema “Ngoja nikapambane na maisha, yakinishinda si ninarudi kwetu tu” na mifano mingine kibao. Kwahiyo mara nyingi tunakuwa tunapambana mguu nje mguu ndani. Katika hali hii, hatuwezi kuwekeza nguvu yetu yote, kwa hali hii ni lazima tutazidiwa na hofu na mara nyingi tutaishia kushindwa. Lakini wale ambao huwa wanaamua kupambana bila kuweka PLAN B, wale ambao kwao neno KUSHINDWA halipo; wale ambao wanajua kabisa watakutana na changamoto na wapo tayari kuzikabili; hawa jamaa siku zote huwa ni washindi.
Karne ya 16, Kiongozi mmoja wa jeshi aliyejulikana kama Cortes aliagizwa kwenda kuivamia nchi ya Mexico. Kamanda huyu alikuwa na wasiwasi kwakuwa jeshi lake lilikuwa dogo na duni sana ukilinganisha na wapinzani wake. Alipomueleza mfalme kuwa jeshi lao ni dogo, mfalme alimjibu “kama hamuwezi kuivamia Mexico na kushinda, basi muuliwe wote na asirudi hata mmoja.” Kamanda Cortes alikuwa akiheshimika sana, na kukataa kuingia vitani kungempunguzia heshima lakini pia kungemsababishia adhabu kwa sababu ya kukataa maagizo ya mfalme. Siku chache baadae, Kamanda Cortes aliwapakia wanajeshi wake kwenye majahazi tayari kuelekea Mexico. Wakati wote wa Safari, alikuwa akipanga mikakati ya kumletea ushindi, alijiambia “NI LAZIMA TUSHINDE AU TUFE”. Wanajeshi wake walionekana wenye wasiwasi sana, haswa wakijua mpinzani wao alikuwa na uwezo mkubwa na jeshi kubwa. Walipofika kwenye fukwe, Kamanda Cortes alitoa amri iliyowashangaza wengi, alimwagiza mmoja wa wanajeshi kuchoma meli. Mwanajeshi yule alipobisha, Kamanda Cortes alimchoma kisu cha shingo na kumuua papo hapo. Baada ya hapo, meli zote zilichomwa moto, kisha Kamanda akawaambia vijana wake; “mmeona tumechoma meli hivyo hakuna namna yoyote ya kurudi nyuma. Uhai wetu kwenye ardhi hii utategemea upambanaji wetu. Lililopo mbele yetu ni moja tu, TUSHINDE AU TUFE.” Baada ya mapambano ya muda, hatumae jeshi dogo lililoongozwa na Kamanda Cortes lilifanikiwa kushinda na kuitawala Mexico.
Ujumbe
Je ni kitu gani unahisi kiliwaongezea nguvu vijana wa Cortes? Ni moja tu, walijua dhahiri hakuna namna nyingine ya kuishi isipokuwa kushinda vita ile. Unapokuwa umejijengea sababu ya kushindwa maana yake umejiandaa kushindwa. Haushindwi kwasababu ya ugumu wa lile jambo, la hasha, unashindwa kwasababu fikra zako haziwi tayari kupambana kwa ukamilifu. Lakini ukifanikiwa kuwekeza fikra zako zote kwenye jambo moja bila kuyumbayumba, bila kusema nikishindwa nitaweka PLAN B, unapata hari na nguvu yakupambana kufanikisha. Unapata nguvu ya kutatua changamoto zinazokukabili ili uweze kufanikisha. Hii haina maana kwamba mambo yatakuwa marahisi, asikidanganye mtu, yatakuwa magumu, tena magumu sana. Lakini ukiwa na nia ya dhati na kuamua kupambana bila kuacha wala kuchoka, mwisho wake utayaona mafanikio. Ili kufanikisha ndoto zetu, tunahitaji kuchoma hilo daraja litakalotushawishi kukimbia mapambano na kurudi nyuma. Unapochoma hilo daraja, unaziaminisha fikra na akili yako kuwa, hakuna kurudi nyuma mpaka utakapofanikiwa. Unapofanya hivi, unaulazimisha mwili na akili kupambana kwa asilimia 120%, unajiweka tayari kupambana na changamoto zozote zitakapokuja.
PIGANIA NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO.
WEWE NI MSHINDI💪💪💪💪💪💪💪💪💪💪
Naam. Hakuna kurudi nyuma ukishachoma meli.