top of page
Search

TAFUTA CHACHU

TAFUTA CHACHU; TAFUTA HAMASA

Huwa napenda kufuatilia interview za watu tofauti tofauti maarufu wakielezea mafanikio yao. Siku moja nilikuwa namfuatilia Donald Trump (raisi wa Marekani kwa sasa), alikuwa anamuelezea rafiki yake mmoja hivi aliyekuwa mjasiriamali. Trump anasema tangia amemfahamu rafiki yake huyo wakiwa wanaanza pilika pilika za kupigania ndoto, hakuwahi kumuona jamaa akikaa daraja la kawaida kwenye ndege. Mara zote alisafiri kwa Business class, daraja la gharama kabisa. Siku moja Trump uvumilivu ulimshinda akaamua kumuuliza rafiki yake huyo, kulikoni bwana wewe na gharama zote hizi, hauogopi kupoteza hela ambayo ungeweza kuwekeza kwenye biashara? Jamaa akamjibu, “ni kweli mimi sio tajiri na natakiwa kuwa na nidhamu ya matumizi. Lakini, kusafiri daraja la juu kuna faida kubwa mbili kwangu; moja, napata nafasi ya kukutana na watu waliofanikiwa na maarufu ambao najifunza kwao mambo mengi lakini pia natengeneza urafiki ambao una faida kibiashara. Na pili, daraja la kwanza linanichochea kutafuta hela kwa uchungu ili nipande tena na tena.”

Ujumbe

Japo mfano wa Trump unaweza kuonekana mkubwa na pengine usilete maana kwa wengi, jibu alilolitoa rafiki yake lina ujumbe mkubwa sana kwetu tunaopigania ndoto zetu. Unajua kwa wengi yetu kuna kawaida ya kuridhishwa na mazingira yanayotuzunguka. Kwa mfano, kama kipato chako ni elfu kumi halafu umezungukwa na watu wenye kipato cha elfu tano, kuna uwezekano wa kuridhika na kujiona umeshafanikisha. Hili jambo linafubaza ndoto za wengi kwasababu wanapoteza ile chachu ya kuendeleza mapambano. Kumbe kuna muda unatakiwa uondoke kwenye yale mazingira uliyoyazoea, uliyozoea kutembelea, ili ukutane na watu watakaokutia hasira ya kuendelea kupambana.

Hata kama unajitahidi kutunza fedha ili kufanya jambo fulani, mara moja moja jaribu kutembelea maeneo ambayo utakutana na watu tofauti na uliowazoea wakutie hasira. Mara moja kwa miezi mitatu, tembelea hotel ya kifahari kunywa hata soda tu pale ukiangalia mpira na watu waliofanikiwa badala kukaa kwenye vibanda umiza siku zote. Badala ya kula kwa mama ntilie, sema siku moja naenda kula kwenye hotel ya nyota tano. Kama umezoea kutembelea bodaboda, mtafute mtu umwombe hata uisogeze gari yake hapa na pale. Baada ya kwenda Coco beach nenda sehemu ambayo inataka gharama. Huduma ya tofauti na ulizozoea utakayoipata itakufanya uongeze nguvu ya kupambana. Kwa kubadilisha mazingira utakutana na watu waliopiga hatua, pengine wakakufumbua macho kuhusiana na mambo fulani ya kibiashara; pengine ukapata marafiki wapya wakapanua biashara yako. Unaweza kuiga hata namna wanavyotoa huduma zao ukaiongezea thamani biashara yako na kuvutia wateja zaidi. Kwenye mapambano yetu ya ndoto ni lazima tuwe na munkari muda wote; na lazima tuwe na moto wa mapambano muda wote. Ukikubali moto ukafifia tu, ghafla ndoto zako zitaanza kufubaa mwishowe utakata tamaa.

Usikubali wewe tu ndio uwe unatembea na bodaboda kila siku; tafuta chachu ya kukufanya ununue gari. Mwombe mtu gari yake uendeshe, akikunyima jitukane kimoyomoyo halafu jiambie “na mimi nitanunua yangu.” Badala ya kwenda kwa mangi kila siku; mara moja na wewe nenda super market kanunue hata pipi kwa elfu moja. Simaanishi uanze kuzuga kwamba ndio maisha yako hapana, ila kwa kufanya hivi kuna kitu kitakuchochea kupambana zaidi, kuna kitu kitakwambia “hata wewe unaweza kuishi maisha haya ukiamua kupambana.” Usikubali kuridhika na hali ndugu zangu, Mungu hajatuumbia umaskini. Achana na zile kauli za kukata tamaa za kusema ooohh kununua gari ni anasa; ooohh kula nyama kila siku ni anasa; ooohhh kuvaa vizuri ni anasa. Haya ni maneno ya kimaskini; ni maneno ya mtu aliyekata tamaa baada ya kushindwa kutungua maembe anasema ni mabichi. Usiseme kupanda ndege ni anasa wakati haujawahi kupanda. Panda kwanza siku moja uone kama haijapambana ili upande tena. Kuna mwandishi mmoja aliwahi kusema, “ukiona wewe ndio bora kuliko wote kwenye kundi lako au jamii yako, ondoka katafute kundi lingine” Pambana uishi maisha mazuri, asikudanganye mtu, hakuna shujaa wa umaskini.

PIGANIA NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO

WEWE NI MSHINDI

Onesmo Mushi

 
 
 

Recent Posts

See All
JE KUNA BAHATI KATIKA MAISHA?

JE KUNA BAHATI KATIKA MAISHA? Oprah Winfrey aliwahi kusema, hakuna bahati kwenye maisha wala hakuna anayefanikiwa kwa kubahatisha....

 
 
 
ANZA NA KIDOGO

KITUMIE KIDOGO ULICHONACHO; MUNGU ATAKUONGEZEA MBELE YA SAFARI Wengi wetu huwa tunazidiwa na hofu na kuogopa kuanza kutembea kuelekea...

 
 
 

1 Comment


Herbert Njama
Herbert Njama
May 14, 2020

Safi sana mkubwa. Maneno mazuri sana haya. Na kwa kweli ndio jambo la maana sana ikiwa unataka kupiga hatua.

Like
Post: Blog2_Post

Subscribe Form

Thanks for submitting!

  • Facebook
  • Twitter
  • LinkedIn
  • Facebook

©2020 by Maabara Ya Maisha. Proudly created with Wix.com

bottom of page