
Untitled
- Onesmo Frank
- May 7, 2020
- 3 min read
USIMWAMBIE MTU NDOTO YAKO
Nikisema hivi huwa nakumbuka sana hadithi ya Joseph katika biblia. Akiwa kati ya watoto kumi na mbili wa mzee Yakobo, Joseph alikuwa akioteshwa na Mungu kwamba atakuja kuwa mtu mkubwa sana, kiongozi ambaye wengi wangekuja kumtegemea. Joseph alioteshwa ndoto mara kwa mara, na kuna wakati mwingine Mungu alimtokea akazungumza nae akiwa usingizini. Joseph akiwa na furaha, alipenda kuwahidithia kaka zake na wazazi wake kuhusu hizi ndoto zinazoonesha maisha yake ya kesho. Kuna siku aliota nyota moja kubwa ikiwa imezungukwa na nyota ndogondogo kibao. Joseph, alipowahadithia kaka zake, walikasirika sana, waliona wivu kwamba huyu bwana mdogo atakuja kuwa mkubwa kuliko sisi na kwamba tutakuwa watumishi chini yake. Joseph alipomhadithia baba yake, baba naye alikasirika, akamwambia “ina maana hadi sisi wazazi wako tutakuwa chini yako?”, hawakupendezwa na ndoto za huyu bwana mdogo.
Wakiwa kwenye malisho ya mifugo siku moja, kaka zake Joseph walizidiwa na wivu na chuki, wakapanga kumuua bwana mdogo. Joseph alipowapelekea kaka zake chakula walipokuwa wanalisha mifugo, walimkamata na kumtupa kwenye shimo kwa lengo la kumuua. Baada ya kusutwa na nafsi, walimtoa kwenye shimo na kumuuza kwa wapita njia kama mtumwa kisha wakadanganya nyumbani kwamba Joseph ameliwa na wanyama wakali. (Unaweza kusoma zaidi kwenye biblia, Mwanzo 37 mpaka 50).
Ujumbe
Hadithi ya Joseph inanikumbusha maneno ya Stanley Nkini, moja kati ya watu ninaojifunza mengi sana kutoka kwake hasa katika mapambano ya kuzifikia ndoto zetu. Stanley sio mtu maarufu au msomi mkubwa, lakini kwenye upande wa maisha na kupigania ndoto, aisee anayo PhD. Tukiwa tunacheza pool-table, Stanley alipenda kusema, “usimwadithie mtu ndoto yako, unaweza kuamka ukakuta ameshaitekeleza.” Naamini Stanley anaitumia falsafa hii katika maisha yake. Ni mpambanaji asiyekata tamaa, mvumilivu na msiri kwenye pilika zake haswa katika kutekeleza ndoto zake. Nadhani Stanley alisoma hadithi ya Joseph au alijifunza kwenye maisha aliyoyapitia mpaka kufika hapo alipo sasa. Katika maisha hauwezi kumuamini kila mtu, kuna watu wengi wasiopenda upige hatua. Hii ni asili ya wanadamu, haswa katika nchi zinazoendelea. Ukimueleza mtu ndoto yako, badala ya kukushauri au kukusaidia kuifikia, atatafuta kila namna kukukatisha tamaa ili usifanikishe. Watu hawa wapo tayari kukupa mifano ya watu walioshindwa kipindi cha nyuma, watakukumbusha umaskini wa familia yako, watakukumbusha elimu uliyonayo, watakufananisha watu fulani na fulani na mengine mengi. Wengine watakutia hofu kwa kukwambia mambo kibao kama vile utapata hasara, utaumwa, utapoteza mtaji, utapoteza marafiki, sijui fulani atakuonaje, sijui jamii itakucheka na mengine mengi sana. Kwa bahati mbaya, kuna muda utakuta hawa jamaa ni watu wako wa karibu sana pengine ni ndugu au rafiki zako. Nadhani Stanley alikuwa analiona hili na kuamua kutushauri kuficha ndoto zetu ili tuweze kuzifanikisha bila kutiwa hofu wala woga. Watu wakifanikiwa kupandikiza hofu na fikra za kushindwa kwenye ubongo wako; kamwe hauwezi kufanikisha ndoto zako kwasababu utayaogopa yote waliyokwambia. Sijui kwanini, ila kuna watu tu huwa hawapendi kuona mtu akipiga hatua, wapo tayari kusubiri ukwame ili waseme “si tulikwambia hatafanikiwa?”, cha ajabu ukifanikiwa watu hawa hawa watakuwa wa kwanza kukupongeza😂. Usiwape nafasi hiyo, washtukize na hatua unazopiga. Simaanishi kuwa usimwamini kila mtu ila kuwa makini kwasababu kaka zake Joseph wamejaa kila mahali, muda wowote wanaweza kuzizika ndoto zako. Ukishawagundua, mapema sana zikikumbatie ndoto zako; kamwe usiwape nafasi. Mwaka 2015, niliwaambia baadhi ya wadau kwamba nataka kutafuta ufadhili wa kwenda Marekani. Kabla hata sijamaliza kuelezea nikaambiwa aaahh wapi, unamjua nani wewe unafikiri ni rahisi. Mwingine akasema “hizo nafasi wanapewaga watoto wa vigogo sio wewe kapuku” na mengine mengi. Nilinyamaza kimya, mada ikaishia hapo hapo. Miezi nane baadae nikawatumia picha nipo New York nakula sandwich.
Penye nia pana njia. Ficha ndoto yako, ipambanie bila kuogopa. Lolote unalolitaka linawezekana.
IPIGANIE NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO
WEWE NI MSHINDI.
Comments