
Untitled
- Onesmo Frank
- May 8, 2020
- 2 min read
KILA UNALOLIFANYA LINA MCHANGO KWENYE NDOTO ZAKO!
Kuna fundi ujenzi mmoja aliyekuwa ameitumikia kampuni yake kwa miaka mingi sana. Baada yakuona kuwa umri umesogea, alimua kuandika barua ya kuomba kustaafu. Kampuni ilisikitika sana kwa kuona kwamba inaelekea kumpoteza mfanyakazi wake mahiri sana. Kampuni ilijibu barua ya fundi kwa kumuomba amalizie kazi moja tu aliyokuwa inatakiwa sana kabla hajaondoka. Fundi huyu hakutaka, alilalamika akaona wanamsumbua na hawaheshimu mchango wake kwa miaka yote aliyofanya kazi. Lakini kampuni ilimsisitiza na kumuomba sana, mwisho alikubali kwa shingo upande. Kampuni ilimnunulia mzee vifaa kibao na kumuomba ajenge nyumba kabla hajaondoka. Kwakuwa mzee hakupenda, aliamua kuwajengea tu ili kuwaridhisha. Alijenga jenga tu nyumba ambayo haikuwa na ubora kama wa kazi nyingine alizowahi kufanya. Alipomaliza ujenzi, siku ya makabidhiano kampuni ilimshukuru sana. Kisha meneja wa kampuni akamwambia fundi, “tunashukuru kwa utumishi wako miaka yote uliyokuwa nasi, kampuni iliamua ujichagulie zawadi kwahiyo hii nyumba ndio zawadi yako” Mzee alitokwa na machozi, akatamani walau angeijenga hii nyumba kwa ubora kama angejua kuwa itakuwa yake, lakini ikawa ameshachelewa. Huo ndio ulikuwa mwisho wa fundi baada ya miaka mingi ya kazi, akizawadiwa nyumba mbovu aliyojenga kwa mikono yake mwenyewe.
Ujumbe
Nilichojifunza kwa huyu fundi ni kimoja tu, “chochote unachokifanya leo, kina mchango kwenye maisha yako ya kesho, kina mchango kwenye ndoto zako”. Kwa bahati mbaya ni vigumu kuona matokeo ya vitu unavyofanya leo kwa miaka mingi ijayo ila kuna kipindi kikifika, huwa tukiangalia nyuma tunaweza kuunganisha dot ya mambo tuliyowahi kuyayafanya. Kwa kiasi kikubwa, maisha tunayoishi leo, hali tuliyonayo leo, ni matokeo ya maamuzi tuliyowahi kufanya kipindi cha nyuma. Kuna uwezekano kwa namna moja au nyingine tulipewa nafasi ya kujijengea nyumba lakini kwasababu hatukujua hii nyumba ingekuja kuwa yetu, tukaijenga kiholela holela. Leo tukiwa ndani kisha nyumba ikawa inavuja, ni kwasababu hatukutekeleza wajibu wetu wa ufundi ipasavyo. Leo nyumba kama imeweka ufa, ni kwasababu tulijiibia sement wenyewe. Leo kama nyumba haina mvuto, ni kwasababu hatukuamua kuipendezesha wenyewe. Kuna fumbo la muhimu sana hapa. Leo kabla haujalaumu upepo kwa kuezua paa; haujalaumu mizizi ya miti kwa kupasua ukuta; kabla haujalaumu bati kuvuja na joto kali kwa sababu ya madirisha madogo; tujiulize kwanza, je, tulitekeleza wajibu wetu ipasavyo tulipopewa kazi ya kujenga??
Mimi baada ya kusoma hii, nimejiuliza maswali matatu; naamini na wewe utaungana nami kujiuliza.Moja, nimetoka wapi? Mbili, Nipo wapi? Na tatu, Ninaenda wapi?
Tukilingundua hili mapema, miaka kumi ijayo hatutalaumu mvua, upepo, mizizi wala majirani.
IPIGANIE NDOTO YAKO; IPAMBANIE NDOTO YAKO
WEWE NI MSHINDI.
Onesmo Mushi
Comments