USIKATE TAMAA
- Onesmo Frank
- May 2, 2020
- 2 min read
Mwaka 1982 nchini Australia, alizaliwa kijana Nick Vujinic. Tofauti na watoto wengine, Nick alizaliwa bila mikono wala miguu. Baada ya baba yake kuona hivi, alinguka karibu kuzimia na mama Nick hakutaka hata kumuangalia mwanaye, alikuwa analia tu kwa uchungu. Wakunga na madaktari wote walipatwa na bumbuwazi, wakasema Nick atakuwa kama majani. Kitu kimoja kizuri, Nick hakuwa na ulemavu wowote kiakili.
Baada ya kukuwa kidogo, wazazi walimpeleka Nick shule lakini alikataliwa wakisema ni mlemavu hivyo apelekwe kwenye shule ya walemavu. Wazazi walikataa na baada ya serekali kubadilisha sheria, Nick aliruhusiwa kusoma kwenye darasa moja na watoto wengine.
Maisha ya Nick shule yalikuwa magumu sana. Alizomewa na wenzake, wengine walimuona kama laana; asiyeweza chochote; mtegemezi na mzigo kwa familia yake. Kutokana na haya, Nick alijaribu kujiua mara kadhaa lakini kuna kitu ndani yake kikawa kinamzuia. Nick alimuomba Mungu usiku na mchana ili miguu na mikono yake iote ili awe kama watoto wengine lakini ilishindikana.
Siku moja mama yake akamleteq gazeti asome kuhusu madaktari bingwa wa watu wenye ulemavu. Baada ya kusoma hili gazeti, Nick alifurahi kujiona hayupo peke yake lakini pia akaona kuwa wapo wenye matatizo makubwa kuliko yake. Nick alibadilika akaikubali hali yake, na kuamua kujifunza mambo mengi yanayofanywa na watu wa kawaida. Nick alijifunza kuendesha baiskeli ya walemavu; alijifunza kuandika vidole vilivyopo kwenye sehemu ya vipande vidogo vya miguu. Nick alijifunza pia kuandika kwa kompyuta; alijifunza kuogelea; kupiga mswaki; kupokea simu na mengine kibao.
Nick alijifunza uhamasishaji na uandishi wa vitabu. Alikuwa na ndoto ya kuwa mhamasishaji na muandishi mkubwa duniani. Tunapoongea sasa, Nick ni mmoja kati ya wahamasishaji kumi wakubwa duniani. Ni bilionea na mtu mwenye mafanikio makubwa duniani. Mwaka 2008, Nick alipata mpenzi ambaye walikutana alipokuja kuhudhuria speech ya Nick. Walifunga ndoa Mwaka 2012 na mpaka sasa Nick ni baba wa watoto wanne, anayeishi maisha ya raha na mafanikio ambayo mimi na wewe bado tunayaota.
Ujumbe
Ndugu zangu, Nick anatufundisha kuwa tusikubali kuyafanya maneno wanayotuambia watu yakawa uhalisia wa maisha yetu. Tusikubali changamoto tunazokutana nazo zikawa kikwazo cha kuzipambania ndoto zetu. Safari ya mafanikio ni ngumu na tutakutana na changamoto nyingi sana na zenye kukatisha tamaa. Kuna muda hata watu tunaowaamini kama ndugu zetu na marafiki zetu ndio watakaokuwa mstari we mbele kutukatisha tamaa; kukwambia hauwezi kwa sababu wewe ni maskini; kukwambia hauwezi kwasababu hauna wazazi; kukwambia hauwezi kwasababu haujalewa au haujaoa; kukwambia hauwezi kwasababu waliokutangulia waliahindwa; kukwambia hauwezi kwasababu umri umeenda sana; kamwe usikubaliane na kauli za hawa watu. Maneno yao yakawe chachu ya mabadiliko; maneno yao yakakuongezee hari ya kuzipambania ndoto zako. Misamiati ya kushindwa, na kukata tamaa uifute kabisa katika kichwa chako. Ukapigane kila kukicha kuyasogelea mafanikio ya ndoto yako; ukapigane kila kukicha kuwaandalia watoto wako kesho yenye thamani; ukapigane kila kukicha ukiwa na imani, nguvu na ni ya dhati ya kuondoka kwenye umaskini. Pale wengine wanapoona changamoto, wewe ukaone fursa. Pale watakapodhani umeanguka na kupotea, wewe ujifunze na kusimama kwa kishindo. Kila siku iendayo kwa Mungu, tuhakikishe tunapiga hatua kuelekea kwenye ndoto zetu bila kujali hiyo hatua ni ndogo kiasi gani.
Nick anatufundisha kuwa penye nia pana njia na tuna uwezo wa kufanikisha lolote lile tukiamua kuamini katika uwezo wetu.
Unaweza kumwangalia Nick Vujinic YouTube kwenye hii link https://youtu.be/l_KZYzTzNjs
Mungu akupe nguvu ya kuzipambania ndoto zako.
Author: Onesmo Mushi
Comments